Mchungaji Dorcas Aahidi Kuwarekebisha Waathiriwa Wa Dawa Za Kulevya
Mke wa Naibu Rais Mchungaji Dorcas Rigathi ametumia fursa leo hii Jumatatu asubuhi kuzuru sehemu za dawa za kulevya katika Kaunti ya Mombasa.
Wakati wa ziara yake Mchungaji Dorcas alitangamana na waraibu wa aina mbalimbali za matumizi ya dawa za kulevya katika maficho yao katika eneo la Shimanzi.
Aliahidi kuwarekebisha wengi wa waraibu ambao wamekubali kwa hiari kurekebishwa.
Wakati wa mwingiliano wake nao, waraibu hao waliahidi kufanya mageuzi mara tu baada ya mchakato wa urekebishaji wengi wakionyesha nia ya kuchukuliwa kupitia mchakato wa ukarabati muafaka kuasi dawa za kulevya.
Mwakilishi wa kike Kaunti ya Mombasa. Zamzam Mohammed ambaye alikuwa ameandamana na Mchungaji Dorcas alitoa changamoto kwa waraibu hao kutekeleza ahadi yao ya mageuzi baada ya wengi kusema wamefukuzwa kazi zao za awali kutokana na uraibu wa dawa za kulevya.
Baadaye Mchungaji Dorcas alitembelea Kituo cha Miritini ambacho ameahidi kuendeleza ukarabati wake ili kuwahudumia waraibu zaidi.
Utafiti wa 2022 wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Pombe na Madawa ya Kulevya NACADA ambao ulitolewa Ijumaa wiki jana ulionyesha kuwa mmoja kati ya Wakenya 6 wenye umri wa miaka 15-65 kwa sasa wanatumia angalau dawa moja za kulevya Hii ina maana zaidi ya Wakenya Milioni 4.7 wameathirika na dawa hizo.
Kuenea kwa pombe za kienyeji katika eneo hilo, kumefikia asilimia7.4 na kuenea kwa pombe kali katika eneo la pwani katika asilimia 4.1.
Pia alikuwepo Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Abdirizak Jaldesa, maafisa wa NACADA na viongozi wengine wa eneo hilo.