Serikali Yalaumiwa Kwa Kuwatisha Walionusurika Kifo Shakahola
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) imeikosoa serikali kuhusu operesheni ya usalama ya Shakahola, ikisema kwamba kukamatwa kwa watu msituni kunawatia hofu manusura.
Akizungumza mjini Malindi wakati wa kikao na wanahabari, Prof. Marion Mutugi, kamishna katika KNCHR ameitaka serikali kuwahakikishia waathiriwa wa Shakahola kwamba watachukuliwa kama walionusurika lakini si washukiwa.
Marion amesema kuwa kuondoa hofu kwa wahasiriwa, kutarahisisha shughuli ya uokoaji kwani manusura zaidi watajisalimisha kwa mamlaka.
Aidha amependekeza mabadiliko ya mkakati katika operesheni ya usalama ili kuzingatia zaidi manusura ambao walikuwa bado wamekwama msituni.
Kwa upande mwingine, amepongeza uongozi wa eneo hilo, Asasi za Kiraia na vyombo vya habari kwa majukumu yao katika janga la Shakahola.
Sambamba na hayo, tume hiyo imezitaka taasisi za kidini kuacha mafundisho yanayoweza kuwadhuru waumini hasa watoto.
Kamishna huyo wa KNCHR ametaka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu shughuli zote za kidini nchini ili kuepusha kujirudia kwa kile kilichotokea katika msitu wa Shakahola.
Kauli ya KNCHR inajiri wiki mbili baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, Aprili 26, kutangaza amri ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri katika shamba la Chakama, ambalo linamiliki msitu wa Shakahola wa ekari mia 800 katika Kaunti ya Kilifi.
Waziri huyo alidokeza kuwa eneo hilo lilitatizika na kwamba amri hiyo ya kutotoka nje itawawezesha maafisa wa usalama kuendelea na shughuli ya uchimbaji na uchunguzi.
Bado katika suala ilo hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani alitangaza mabadiliko makubwa ya wakuu wa polisi katika Kaunti ya Kilifi mnamo Aprili 28.
Kindiki alisema kuwa uhamisho wa wakuu wa polisi utawezesha serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola kaunti hiyo.
Kufikia jana Jumatano, Mei 10, takriban miili 145 ilikuwa imefukuliwa msituni.