Timu Ya Rais Ruto Yakubali Anayodai Raila.
Kamati ya watu 14 ya pande mbili inayojumuisha muungano wa Azimio la umoja one-kenya na Wabunge wa Kenya Kwanza leo hii Jumatano ilikubali kuheshimu matakwa ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Mrengo wa Kenya Kwanza wa Kamati ya Vyama Viwili umekubali uamuzi wa Raila kwamba mazungumzo yakamilishwe ndani ya siku 30 na nyongeza ya siku thelathini iwapo wanachama hao watashindwa kufikia uamuzi kwa wakati.
Kamati hiyo Ikihutubia wanahabari katika ukumbi wa Bomas of Kenya, imebaini kuwa wako tayari kuendelea na mazungumzo, na iwapo kutakuwa na haja ya kuongeza muda, watatoa taarifa kwa taifa.
Hapo awali, kikosi cha Kenya Kwanza kilipinga vikali makataa ya siku 30, na kuyataja kuwa mafupi mno kwa mazungumzo ya maana na Upinzani.
Kulingana na Seneta Mteule wa Kenya kwanza Esther Okenyuri muungano huo ilijitolea kuweka masilahi ya Wakenya, sio viongozi mbele na itakuwa hatua mbaya iwapo watasusia mazungumzo ya pande mbili
Mnamo Jumatatu, Mei 8, Raila alionya kwamba ataongoza wafuasi wake kurejea katika maandamano iwapo mazungumzo hayo yatapita siku 30.
Kiongozi huyo wa Chama cha (ODM) pia alimpa Rais William Ruto masaa 48 kwa upande wake kufika mezani kwa mazungumzo.
Kamati hiyo pia ilikubali kwa kauli moja kutofanya pingamizi za awali ambazo zilikuwa zimewasilishwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Kanini Kega, akitaka Chama cha Jubilee kujumuishwa katika mazungumzo yanayoendelea.
Katika barua aliyoiandikia Kamati ya Vyama viwili, Kega alishangaa ni kwa nini Chama cha Jubilee kiliachwa bila mwakilishi ilhali ni mojawapo ya vyama vikuu vya kisiasa nchini.