Safari-Link Kusitisha Safari Zake Za Kitale
Kampuni ya usafiri wa ndani ya Safarilink itasimamisha shughuli zake kutoka Nairobi-Kitale mwezi ujao, mwaka mmoja tu baada ya kuanzisha upya safari za ndege, ikitaja kupata hasara kibiashara na miundombinu.
Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Alex Avedi amesema hatua hiyo imetatizwa na gharama kubwa ya mafuta na uhaba wa vifaa vya ndege, hivyo kulazimika kusitisha safari za ndege.
Shirika hilo, ambalo kwa sehemu kubwa husafiri maeneo ya watalii, lilisema safari ya mwisho itakuwa Juni 8.
Ndiyo shirika pekee la ndege la ndani katika linalosafiri mara tano kwa wiki kwa kutumia ndege ya Dash 8-100/200.
Avedi amesema shirika hilo la ndege lilikuwa likipitia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na bei ya mafuta, viwango visivyofaa vya kubadilisha fedha na miundombinu duni ya viwanja vya ndege.
Wateja ambao walikuwa wameweka tikiti kuanzia tarehe 9 Juni watarejeshewa pesa zote.
Safarilink ilizindua shughuli zake kwenye njia hiyo mwaka wa 2016. Safari hizo za ndege zilisitishwa mwaka wa 2020 kwa miaka miwili ili kupisha njia ya ukarabati katika uwanja huo wa ndege.
Shirika hilo la ndege lilianza tena kufanya kazi mwaka jana.