Khalwale Kwa Raila: Tuko Tayari Kwa Mazungumzo
Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amemjibu kiongozi wa Upinzani Raila Odinga akisema muungano tawala wa Kenya Kwanza uko tayari kwa mazungumzo.
Katika akaunti yake ya Twitter, Khalwale amesema muungano wa Kenya Kwanza unasalia mwaminifu katika mazungumzo ya pande mbili zinazoongozwa na bunge ili kumaliza mzozo wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na Odinga.
Odinga alitishia jana Jumatatu kwamba muungano huo hautasita kuanzisha tena maandamano ikiwa mazungumzo yaliyokwama hayatarejelewa kufikia kesho Jumatano.
Kiongozi huyo alisema ameonyesha nia njema kwa kusitisha maandamano ya kuunga mkono mazungumzo yaliyoanzishwa na rais lakini hatakuwa na chaguo lingine kama hatua haitachukuliwa ila kuitisha maandamano tena.
Muungano wa Azimio ulikuwa umepanga kufanya maandamano mengine Alhamisi wiki jana lakini ulisema katika taarifa ya uongozi wake kwamba umekubali kusitisha hatua hiyo.
Wafuasi wa Odinga wamefanya maandamano kadhaa tangu Machi kwa madai kuwa kura ya urais mwaka jana iliibiwa lakini pia kwa kile anachosema ni kushindwa kwa serikali kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha.