Baadhi Ya Wakenya Waliokwama Sudan Wamewasili Nairobi
Kundi la kwanza la wakenya kutoka Sudan waliokumbwa na vita waliwasili nchini kwa ndege ya kijeshi jana Jumatatu Jioni.
Kundi hilo lilikuwa na wanafunzi 39, kati yao Wakenya 19, Wasomali 19, na raia mmoja wa Saudi Arabia.
Walipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Jomo Kenyatta jijini Nairobi na Waziri wa Ulinzi Aden Duale.
Duale alisema wanafunzi hao walisafiri kwa barabara hadi Sudan Kusini ambako walipanda ndege hiyo ya kijeshi, na kuongeza kuwa Wakenya zaidi walikuwa wameratibiwa kusafirishwa kwa ndege.
Kuwasili kwao kulijiri saa chache kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kutangaza kwamba pande zinazozozana za Sudan zilikubali kusitishwa kwa mapigano kwa saa 72.
Blinken alisema Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Vikosi vya RSF yalikubaliana baada ya mazungumzo makali ya saa 48.
Usitishaji wa mapigano utaanza saa sita usiku mnamo Aprili 24.
RSF ilisema katika taarifa yake kwamba imekubali kusitisha mapigano “ili kufungua njia za kibinadamu, kuwezesha harakati za raia na wakaazi, kuwawezesha kutimiza mahitaji yao, kufikia hospitali na maeneo salama, na kuhamisha misheni ya kidiplomasia.”
Takriban watu 427 wamethibitishwa kuuawa na zaidi ya 3,700 kujeruhiwa, shirika la habari la AFP liliripoti Jumatatu, likinukuu mashirika ya Umoja wa Mataifa.