Home » NTSA, Polisi Kushirikiana Kudhibiti Ajali

Mamlaka ya Usalama barabarani (NTSA) na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) wameanzisha msako wa pamoja dhidi ya magari yasiyofuata sheria na kampeni ya uhamasishaji inayolenga kuzuia ongezeko la ajali za barabarani wakati wa likizo hii ya Pasaka.

 

Msako mkali uliofanyika Makuyu kwenye barabara kuu ya Nyeri ulishuhudia zaidi ya magari 50 yakiwa yamekamatwa kwa kukiuka kanuni za trafiki.

 

Wakati wa msako huo ulioongozwa na mkuu wa NTSA kanda ya Kati Bora Nguyo, aligundua kuwa magari mengi hayakufaa barabarani, huku mengine yakipatikana yakiwa na madereva wa mwendo kasi.

 

Bora amesema ajali nyingi za barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu kwa kushindwa kuzingatia sheria za barabarani na kuwataka madereva kuwa waangalifu zaidi wanapokaribia barabara yenye utelezi wakati huu wa mvua.

 

Vile vile amesema Usalama barabarani bado ni jukumu la pamoja kati ya watumiaji wote wa barabara wakiwemo abiria na wale wanaotembea kwa miguu.

 

Madereva waliohojiwa walisema kuwa msako huo utasaidia katika kupunguza ongezeko la ajali.

 

Maafisa wa Chama cha Usalama nchini Kenya wakiongozwa na mwenyekiti wake David Kiarie walitoa wito wa kuondolewa kwa Mkurugenzi Mkuu wa NTSA George Njao ambaye walimshutumu kwa kutofanya lolote huku mauaji ya barabarani yakiendelea kushuhudiwa.

 

Kiarie amelaumu ajali mbaya za hivi majuzi kutokana na kushindwa kwa Mamlaka kutekeleza kanuni za ukaguzi wa magari, akibainisha kuwa magari mengi yaliyohusika yalikuwa na hitilafu ya breki.

 

Akirejelea ajali ya Jumamosi katika mji wa Migori iliyohusisha lori lililokuwa likisafirisha mchele liliwagonga watu na kusababisha vifo vya takriban watu wanane na nyingine moja wiki jana iliyohusisha basi la Chuo Kikuu cha Pwani na matatu huko Naivasha ambapo watu 20 waliuawa….Kiarie amesema ajali hizo zingeweza kuepukika iwapo magari hayo yangefanyiwa ukaguzi wa kawaida.

 

Watu elfu 1,072 wamefariki kati ya Januari na Machi mwaka huu.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!