Wapangaji Waamriwa Kuondoka Kwenye Jengo La Thindigua
Serikali ya Kaunti ya Kiambu na timu ya Sekta mbalimbali kuhusu Ujenzi wa Majengo wameamuru wapangaji wa jengo la ghorofa tano katika eneo la Thindigua Estate kuondoka mara moja.
Jengo hilo limekuwapo kwa miaka 10 sasa ila limeanza kutengeneza nyufa kwenye kuta ambazo zilifichua udhaifu wa muundo huo.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Kaunti, Idara ya Ardhi, Nyumba na Mipango ya Kiufundi Salome Muthoni Wainaina alisema walipokea simu asubuhi kuhusu jengo linalozama katika Eneo hilo ambapo alihusisha timu ya Sekta mbalimbali ili waweze kubaini sababu.
“Tumefikia uamuzi, kwa kushirikiana na programu zetu zingine za usalama ambazo ziko hapa kwamba wapangaji wote wanapaswa kuondoka kwenye nyumba hizo leo.” Alisema
Kumeripotiwa visa vya kuporomoka kwa majengo katika Kaunti ya Kiambu na kusababisha vifo na majeruhi huku kukiwa na madai ya ushirikiano kati ya wamiliki na maafisa wafisadi wa kaunti.