Mwanamke,22, Apigwa Na Umeme Hadi Kufa
Mwanamke mwenye umri wa miaka 22 alipoteza maisha Jumapili katika kisa kinachoshukiwa cha kunaswa na umeme katika mtaa wa Kilimani Nairobi.
Kulingana na ripoti ya polisi, alikuwa pamoja na marafiki zake tukio hilo lilipotokea.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 22 alipatikana bafuni akiwa amelala sakafuni, dakika chache baada ya kujitoa kwenye karamu kwenda kuoga.
Wakiwa bafuni, marafiki zake walisema walimsikia akianguka na kumwita lakini hawakupata majibu yoyote.
Mara moja wakakimbilia bafuni, wakavunja mlango na kumkuta amejilaza akiwa ameshikilia bomba la kuogea.
“Alikuwa ameshika bomba la kuoga katika mkono wake wa kulia ambao pia ulikuwa na michubuko ya moto kwenye kidole cha kwanza. Pia alikuwa na michubuko kifuani,” ripoti ya polisi ilibainisha.
Alikimbizwa katika hospitali ya karibu lakini alitangazwa kuwa amefariki alipofika.
Maafisa hao walisema wanafanya uchunguzi zaidi kubaini chanzo cha kifo cha msichana huyo mwenye umri wa miaka 22.