Waziri Wa Ulinzi Aden Duale Avunja Ukimya Wake Kuhusu Maandamano Ya Azimio

Waziri wa Ulinzi Aden Duale amevunja ukimya wake kuhusu maandamano yanayoendelea ya Azimio la Umoja One-Kenya.
Duale anasema maandamano hayo yamechochewa na maslahi ya kibinafsi ya kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga, madai ambayo waziri mkuu huyo wa zamani alikanusha hapo awali.
Akiongea kwenye Radio moja humu nchini ,Duale amesema Odinga anafaa kujitokeza wazi kuhusu anachotaka.
Waziri huyo amependekeza kuwa muswada wa baada ya uchaguzi wa 2007/2008 ulikuwa ukivuta upande wake, akidai Odinga alimshurutisha rais wa wakati huo Mwai Kibaki katika mazungumzo ambayo hatimaye yalipelekea serikali kuu ya muungano.
Ikumbukwe kwamba kwa sasa viongozi wa Azimio la Umoja one-Kenya wanafanya maandamano ya kila wiki -Jumatatu na Alhamisi – kushinikiza utawala wa Rais William Ruto kupunguza gharama ya maisha, miongoni mwa masuala mengine.
Duale amesema kurejeshwa kwa ruzuku kwa mafuta na bidhaa za chakula kama vile unga wa mahindi sio suluhisho la haraka la changamoto za maisha ambazo Wakenya wanakabili.
Waziri huyo ameendelea kudai kuwa Odinga alikuwa akipata ufadhili wa maandamano hayo kutoka kwa watu wengine, haswa familia yenye nguvu nchini Kenya.
Odinga, katika hotuba zake za maandamano, anadai Rais Ruto alihujumu matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022, na kwa hivyo yuko ofisini “bila utaratibu”.
Aidha vile vile Anaitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuipa timu ya Azimio ufikiaji wa data za kielektroniki za utumaji wapiga kura.
Kuhusu jukumu la Kenya katika ulinzi wa amani wa DRC, Waziri wa Ulinzi Duale amesema ilikubaliwa katika mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki kwamba Kenya inapaswa kuchukua nafasi ya kwanza katika kurejesha utulivu, haswa mashariki mwa DRC, ambayo iko chini ya udhibiti wa waasi wa M-23.