Picha Ya Rais William Ruto Yaanguka Alipowasili Mkutano Nairobi

Picha ya rais William Ruto ilianguka katika Hoteli ya Ole Sereni jijini Nairobi leo hii Alhamisi, muda mfupi baada ya kuwasili kuongoza Kongamano la Wafanyabiashara wa Marekani.
Mkuu huyo wa nchi ambaye alifika kituoni hapo saa nane alasiri, alikuwa bado hajaingia kwenye ukumbi wa mikutano, tukio hilo lilipotokea.
Baada ya picha hiyo kuanguka kutoka ukutani, haikurejeshwa katika nafasi yake mara moja kwa sababu ya skrini kubwa chini ya eneo lake la asili ambayo ilikuwa ikizuia urekebishaji wa haraka.
Waandaaji wa mkutano, hata hivyo, walipata njia ya kuirekebisha kwa kutumia ngazi ya muda, dakika kadhaa baadaye.
Tukio hilo limeleta mkanganyiko kwa waandaaji wa mkutano kwani kwa kawaida ni utamaduni wa heshima kuwekwa picha ya rais wakati wowote anapokuwa, haswa katika shughuli rasmi.
Mkutano wa Biashara wa AmCham ni jukwaa la kimkakati la kuimarisha biashara na uwekezaji wa njia mbili kati ya Marekani na Afrika Mashariki.
Mkutano huo unalenga kuziwezesha kampuni binafsi kuendesha mahusiano ya kiuchumi ya muda mrefu, kuimarisha biashara na kukuza uwekezaji.
Kuhudhuria kwa Ruto katika Mkutano wa AmCham kulikua tukio la kwanza rasmi ambalo alikuwa akiandaa Alhamisi, Machi 30 baada ya kurejea Kenya kutoka kwa ziara yake ya siku nne nchini Ujerumani na Ubelgiji.