Home » Rais Ruto, Wabunge Wamuomboleza Mbunge Maalim Hassan

Rais William Ruto ameomboleza kifo cha Mbunge wa Banissa Kulow Maalim Hassan, ambaye aliaga kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya ajali siku ya Jumamosi.

 

Mbunge huyo alifariki Jumatano asubuhi katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

 

Katika ujumbe wake Jumatano, Rais William Ruto amewapa pole wakazi wa Banissa kwa kumpoteza mbunge wao.

 

“Natuma rambirambi zangu kwa familia, wafanyakazi wenzangu na marafiki. Tumempoteza mtumishi wa umma aliyejitolea na mtetezi mwenye shauku kwa watu na masilahi ya Kaunti ya Mandera kwa jumla,” Ruto rambirambi.

 

Waziri wa ulinzi Aden Duale na mbunge wa Mvita Mohamed Soud Machele pia wametuma risala zake za rambirambi kwa wapiga kura wa Banissa na familia ya marehemu mbunge huyo.

 

Vile vile Mbunge wa Mandera Magharibi Adan Haji Yussuf ameomboleza Kulow kama kiongozi mkuu na Muislamu aliyejitolea ambaye alicheza jukumu muhimu katika jamii.

 

Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Esther Passaris pia ameipa pole familia ya Kulow na eneo bunge lake.

 

Mbunge huyo alikuwa akihudumu muhula wake wa pili.

 

Mwaka 2017 aliingia bungeni kupitia tiketi ya chama cha Economic Freedom Party (EFP) na mwaka 2022 alitetea kiti chake kupitia United Democratic Movement (UDM).

 

Mnamo Machi 20 alikuwa Mandera ambako kulikuwa kunazinduliwa ripoti ya hali ya afya katika kaunti hiyo.

 

Ameacha wajane watatu na watoto 16.

 

Atazikwa jijini Nairobi kwa kufuata kanuni za dini ya Kiislamu.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!