Gachagua Akutana Na Makatibu Wakuu Walioambatanishwa Na Ofisi Yake
Naibu Rais Rigathi Gachagua leo hii Jumatatu asubuhi alikutana na Makatibu Wakuu wa Tawala (CAS’s) walio katika ofisi yake.
Makatibu hao ni pamoja na Ann Wanjiku Mwangi, Edwin Sudi Wandabusi na Nicholas Ngabiya Rioba.
Gachagua alisema makatibu waliripoti ofisini kwake Alhamisi iliyopita, mara tu baada ya kuapishwa katika Ikulu.
Makatibu hao walisema majukumu yao yatakuwa ni Uhusiano na Tume za Kikatiba na Ofisi Huru katika masuala yanayohitaji uingiliaji kati wa serikali ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na bajeti, uundaji wa sera, na utekelezaji wa mapendekezo yao.
Pia, makatibu hao watakuwa wanaratibu upangaji na kusimamia utekelezaji wa programu na miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo; Kusimamia Marekebisho ya Sekta ya Umma na kazi nyingine yoyote kama atakavyoagizwa na Rais.
Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu iliwazuia makatibu wote 50 walioteuliwa kuwa ofisini kusubiri kuamuliwa kwa ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria wa Kenya LSK na Taasisi ya Katiba.
Jaji Hedwig Ong’undi pia aliwazuia kwa muda walioteuliwa kupata mshahara, malipo au manufaa yoyote.
Kupitia kwa wakili Dan Okemwa, LSK na Katiba zilisema uteuzi huo unaenda kinyume na barua kwa mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma kutoka kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Oktoba mwaka jana akiomba kutangaza nafasi za kazi 23 katika afisi ya makatibu wakuu.
Naibu rais Gachagua ndiye anayeongoza nchi huku Rais William Ruto akiwa katika ziara ya siku nne ya nchi za kigeni nchini Ujerumani na Ubelgiji kwa mazungumzo ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili.