Home » Viongozi Wa Kenya Kwanza Wadai Raila Odinga Anafadhiliwa Kufanya Maandamano

Viongozi Wa Kenya Kwanza Wadai Raila Odinga Anafadhiliwa Kufanya Maandamano

Mbunge wa Thika mjini Alice Ng’ang’a anadai kuwa kinara wa upinzani Raila Odinga alilipwa Ksh BILIONI.10 ili kuchochea machafuko dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.

 

Kulingana na mbunge huyo, wafadhili akiwemo kiongozi mashuhuri ambaye hakumtaja, wamefadhili juhudi za Raila za kuleta machafuko nchini kupitia maandamano makubwa.

 

Ng’ang’a alizungumza hayo katika Kanisa Kuu la A.I.P.C.A Thika leo hii Jumapili wakati wa ibada ya shukrani kwa Waziri wa Biashara Moses Kuria.

 

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi, wabunge Martha Wangari wa (Gilgil), Jane Kihara wa (Naivasha), Patrick Munene wa (Chuka Igamba Ng’ombe), John Njuguna wa (Kiambaa), Geoffrey Wandeto wa (Tetu), Maina Karobia wa bunge la afrika mashariki (EALA), Rahab Mukami wa(Nyeri) na Anne Muratha wa (Kiambu).

 

Mbunge huyo amedai kuwa serikali inafahamu shughuli hiyo na ina ushahidi wa mahali ilipofanyika, na kwamba wana hata picha za kiongozi huyo wa ODM na wafadhili wake.

 

Amesema wafadhili wanapaswa kutoka katika maficho yao na kutangaza maslahi yao katika kuyumbisha serikali na uchumi wa nchi.
Mwenzake wa Naivasha, Jane Kihara, amemshutumu Rais wa zamani Uhuru Kenyatta kwa kuwa nyuma ya maandamano makubwa ya viongozi na wafuasi wa Azimio.

 

Wakati uo huo, waziri Kuria amemtaka Rais huyo wa zamani kufuata nyayo za watangulizi wake Daniel Moi na Mwai Kibaki kwa kustaafu kwa amani na bila kuingilia utawala wa sasa.

 

Kuria alidai kuwa Uhuru amejificha nyuma ya Raila ili kuunda vizuizi kwa tawala wa rais Ruto.

 

Wiki iliyopita, kinara wa upinzani Raila Odinga alitangaza kuwa maandamano hayo yatafanyika Jumatatu na Alhamisi kila wiki hadi serikali itakapopunguza makali ya maisha.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!