Nyota Wa Zamani Wa Ujerumani Mesut Ozil Astaafu
Nyota wa soka duniani Mesut Ozil amestaafu. Kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid na Arsenal alikuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Ujerumani kilichoshinda Kombe la dunia nchini Brazil mwaka wa 2014.
Ozil amestaafu soka akiwa na umri wa miaka 34.
Mchezaji huyo wa ujerumani mwenye asili ya Uturuki alistaafu katika kikosi hicho mwaka wa 2018 huku kukiwa na mjadala wa kisiasa nchini Ujerumani kuhusu ongezeko la wahamiaji haramu na kisha kupiga picha na rais wa uturuki Tayyip Erdogan na kusema alikabiliwa na “ubaguzi wa rangi na ukosefu wa heshima” juu ya asili yake ya Kituruki.
“Nimekuwa na fursa ya kuwa mchezaji wa kimataifa kwa takriban miaka 17 , kwa sasa nashukuru sana kwa nafasi hiyo ya kusakata mpira,” Ozil, ambaye hivi majuzi aliichezea timu ya Uturuki ya Istanbul Basaksehir, alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wake wa Instagram na facebook.
“Lakini katika miezi ya hivi karibuni, nimesumbuliwa majeraha, hili lilikuwa dhihirisho wazi kuwa ni wakati wa kuondoka kwenye hatua kubwa ya soka.”
Ozil alicheza mechi 645 kwa klabu na Taifa, na kufunga mabao 114
Alianza maisha yake ya soka akiwa na Schalke 04 nchini Ujerumani, kabla ya kuhamia Werder Bremen. Uchezaji wake ulimfanya aitwe kwenye kikosi cha Ujerumani kwa Kombe la Dunia la 2010, ambapo aliisaidia nchi yake kufika nusu fainali.
Alisajiliwa na Real Madrid mwezi mmoja baada ya Kombe la Dunia na alikaa miaka mitatu nchini Uhispania, akishinda taji moja la LaLiga na Kombe la Super Cup la Uhispania. Ozil alicheza mechi 105 za LaLiga akiwa na Real, akifunga mabao 19.
Alijiunga na Arsenal mwaka wa 2013, na kuisaidia kushinda taji la kwanza kati ya manne ya Kombe la FA mwaka uliofuata. Alifunga mabao 33 ya Premier League na kutoa pasi za mabao 59 katika wakati wake Arsenali.
Ozil alijiunga na Fenerbahce ya Uturuki mwaka 2021 baada ya Arsenal kusitisha mkataba wake na kisha kuhamia Istanbul Basaksehir chini ya mwaka mmoja baadaye.
“Imekuwa safari ya kufana iliyojaa na hisia zisizoweza kusahaulika,” aliongeza.
“Nataka kushukuru vilabu vyangu – Schalke 04, Werder Bremen, Real Madrid, Arsenal FC, Fenerbahce, Basaksehir na makocha walioniunga mkono, pamoja na wachezaji wenzangu ambao wamekuwa marafiki.
“Sasa ninatazamia kila kitu kilicho mbele yangu akiwemo mpenzi wangu, Amine, na mabinti zangu wawili wazuri, Eda na Ela.”