UDA Wataka Odinga Akamatwe Kwa Kuendesha Maandamano Ya Vurugu
Wabunge kutoka chama tawala cha UDA sasa wanataka muungano wa Azimio la Umoja kuwajibikia uharibifu ulioshuhudiwa wakati wa maandamano makubwa yaliyofanyika Jumatatu.
Katika taarifa siku ya Jumanne, Kenya Kwanza ilieleza kuwa maandamano yaliyoongozwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga yalisababisha hasara kubwa ya uvamizi wa uporaji wa mali ya Umma kinyume na ilivyokuwa imejatwa.
Walimshutumu Bw. Odinga kwa kuratibu ghasia hizo ambazo wanasema kwa kiasi kikubwa zililemaza shughuli za biashara na huduma nyingine za umma. Wanasema sasa itailazimu serikali kutumia mabilioni ya pesa katika kurekebisha na kukarabati jiji.
‘Hasara na uharibifu uliotokana na shughuli za machafuko za Bw. Odinga zilileta hasara ya mabilioni ya pesa,” walisema.
Wabunge hao sasa wanataka asasi za usalama kuanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo na kuwafikisha wahusika wote mahakamani.
“Tunawaomba mtekeleze sheria kwa uthabiti na kuwawajibisha wahusika wote wa ghasia ya uhalifu iliyotekelezwa kwa amri ya Bw. Odinga,” walisema wabunge wa UDA.
“Lazima watozwe kwa kila jiwe linalotupwa, mali iliyoporwa, bidhaa zilizoharibiwa na watu waliojeruhiwa.”
Sambamba na hilo, wanataka Bw Odinga achunguzwe ili kubaini iwapo alikiuka sheria, wakisisitiza kwamba hapaswi kuruhusiwa kufanya kazi zaidi ya maagizo ya katiba na iwapo atapatikana na hatia, anapaswa kuhukumiwa.