Mandonga ‘Mtu Kazi’ Arejea Kenya Na Ngumi Ya Mlungambuga

Mwanamasumbwi raia wa Tanzania Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ ametangaza hali ya hatari kwa bondia maarufu wa Uganda, Kenneth Lukyamuzi atakayepambana naye Machi 25 kwenye Ukumbi wa KICC, jijini Nairobi, Kenya.
Akizungumza jijini Mwanza katika hafla ya uhamasisho wa usalama barabarani, Mandonga Mtu Kazi amesema pambano hilo la kukata na shoka, litakuwa la kumzamisha mpinzani wake Lukyamuzi
Mandonga ametangaza atakuwa akiwasili Nairobi na Ngumi ya Mlungambunga kutoka jangwa la sahara kwenye upepo mkali.
Amedai iwapo ngumi ya Mlungambunga litamkuta mganda, basi ataelekea moja kwa moja jongomeo akiwa anapepea.
“Waafrika wote wajiandae kushuhudia mtu akisulubiwa ulingoni siku hiyo mubashara ndani ya runinga,” alisema Mandonga huku akisisitiza watamchapa mpinzani wake mapema sana kwa ‘knock out’ .
“Nimefurahi sana kwa kukubaliwa pambano hili kuonyeshwa mubashara kwenye runinga, hii italifanya lionekane kote Afrika. Huu ni wakati wa kuionyesha Afrika na dunia kuwa Mandonga ni mtu kazi kwelikweli. Naenda kutuma salamu. Kama kuna bondia yeyote anayejiamini aje mimi kazi yangu ni moja tu – kumchapa!” Kasema Mandonga.
Kabla ya pambano hilo , bondia Nick Otieno wa Kenya atakichapa na Hassan Ndongo wa Tanzania.
George Bonabucha wa Tanzania atavaana Michael Diares wa Afrika Kusini na mwanandondi wa kike Fatuma Yazidu wapigane na bondia wa Uganda.