Zuchu Na Baraka Za “Napambana” Kwa Wanawake

Siku ya wanawake duniani itafanyika siku ya Jumatano tarehe 8 Machi na bila kusahau changamoto wanazopitia wanawake katika harakati za maisha, msanii kutokea lebo ya WCB Wasafi Zuchu, amewabariki mashabiki wake na kibao alichokipa jina la “Napambana”
Napambana ni jiwe lingine kutoka kwa mwandishi huyu mwenye mashairi matamu ya mtindo wa Baibuda yanayoelezea pilika pilka za wanawake katika kusaka tonge la kila siku kwa kujitoa na kufanya kazi za hatari zaidi katika mishemishe za kupata kipato.
Sambamba na wimbo wenyewe pia, Zuhura ameachia video ya wimbo huo ikionesha mikasa wapitiayo wanawake ikiwemo kuuza miili yao, kufanya kazi za ukondakta, kuuza vyuma chakavu pamoja na makopo ili tu waweze kuendesha familia zao ambazo wanawake wameonekana kama tegemeo.
Hii ni ngoma ya kuwatia moyo wanawake ambao wamekuwa uti wa mgongo wa familia zao wazidi kujitoa na kusonga mbele zaidi kwa kuwa riziki mafungu saba.
Huu ni wimbo wa pili mwaka huu kuachiliwa na Zuchu baada ya ngoma ya Utaniua huku upande wa Audio mixing imepitia katika mikono ya Lizer Classic kutolea WCB Wasafi na video ikifanywa na director Folex.