Seneta Osotsi Adai Uamuzi Kuhusu Irene Masit Ulipangwa
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi amedai kuwa uamuzi uliotolewa na mahakama inayomchunguza kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Irene Masit ulikuwa umepangwa.
Haya yanajiri baada ya jopokazi linaloongozwa na jaji Aggrey Muchelule kusema Jumatatu kwamba madai ya utovu wa nidhamu uliotolewa dhidi ya Kamishna Masit yalithibitishwa kwa kiwango kinachohitajika na kwamba yafaa afurushwe.
Kulingana na jopo hilo, Masit alikubali pendekezo la maajenti wa muungano wa Raila Odinga Azimio La Umoja-One kenya la kukagua matokeo ya uchaguzi wa urais na kulazimisha marudio.
Akiongea kwenye kipindi cha runinga moja humu nchni, Seneta Osotsi ameteta kuwa uamuzi huo ulitarajiwa akidai kuwa jopo hilo linatenda kwa mujibu wa matarajio ya serikali.
Seneta huyo wa Vihiga ameendelea kudai kuwa kuna uhusiano wa kifamilia kati ya Mucheule, aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, sababu zaidi ya kuthibitisha kuwa uamuzi huo haungeweza kuporomoka zaidi kutokana na kumtimua kamishna Masit.
Vile vile, ametoa maoni kuwa jopo hilo lingetumika tu kama njia rasmi ya kumtimua Masit na wanachama wengine wa makamishna wa ‘Cherera Four’ ambao walijiuzulu kabla ya vikao vya jopo hilo kuanza.
Rais William Ruto kwa wakati huo ametangaza nafasi zilizoachwa wazi katika bodi ya uchaguzi, na hivyo kutoa mwanya kwa uajiri wa makamishna wapya kuanza.
Kupitia Notisi ya Gazeti la Februari 27, 2023, Ruto ameteua jopo la uteuzi wa wanachama saba, wiki mbili baada ya kutangaza nafasi zilizoachwa wazi katika baraza la uchaguzi.
Jopo la Uteuzi litajumuisha wawakilishi wa Tume ya Huduma za Bunge, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Kisiasa (PPLC), Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), na Baraza la Dini Mbalimbali la Kenya.