Home » Serikali Yapiga Marufuku Matumizi Ya Bunduki Kwa Wafugaji

Sasa itakuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutumia bunduki kuchunga mifugo yake.

 

Rais William Ruto jana Jumapili ametoa agizo hilo la kupiga marufuku mifugo na kuwaambia wafugaji kutumia silaha zingine kuchunga mifugo wao.

 

Agizo lake linajiri wakati baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa Kenya yakikumbwa na mashambulizi ya hapa na pale kutoka kwa majambazi ambao wameua wenyeji na kuiba mifugo.

 

Utumiaji wa silaha kali kama vile bunduki miongoni mwa jamii za wafugaji umekuwa ni jambo la kawaida hasa kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya wafugaji kujikinga na mifugo yao wanaposhambuliwa na majambazi au wanyama pori.

 

Katika matukio mengi hata hivyo, bunduki zizo hizo zimetumika kuwatisha wengine wanapoiba mifugo miongoni mwa jamii.

 

Rais Ruto ambaye alikuwa akizungumza mjini Lamu alisema serikali imetenga shilingi bilioni 20 ili kukabiliana na ukosefu wa usalama, na akasisitiza msukumo wake wa kutaka bunduki zote ambazo hazina leseni mikononi mwa raia zikabidhiwe kwa polisi.

 

Katika maeneo kama vile Bonde la Suguta, Kapedo, Tiaty Arabal, Kainuk, wafugaji hawawezi kuhama kutoka eneo moja hadi jingine kutafuta malisho bila bunduki zao kwa kuhofia usalama.

 

Wakati uo huo huko Samburu, mamia ya watu sasa wamekita kambi eneo la Loiborngare baada ya kutoroka makwao. Akina mama hawa, watoto na wazee wote wanatoka Porra arae ambako mashambulizi ya majambazi yalikuwa yamekithiri.

 

Kulingana na mbunge wa eneo hilo zaidi ya familia mia 300 kwa sasa zinatafuta makazi mbadala. Shule tatu huko Porra, Sepei na Lkek-puki zimesalia kufungwa kufuatia mashambulizi hayo.

 

Watu waliokimbia makazi yao wanaitaka serikali kuhakikisha kuna usalama wa kutosha huko Porra ili kuwawezesha kurejea makwao.
Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda ambaye aliwapa watu waliokimbia makazi yao chakula anataka serikali kushughulikia masuala ya ukosefu wa usalama ipasavyo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!