Viongozi Narok Watoa Hoja Kali Kuhusu Uhifadhi Wa Msitu Wa Mau
Aliyekuwa Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel ole Kenta ametoa wito kwa Waziri wa Mazingira na Misitu Soipan Tuya kutetea uhifadhi wa Msitu wa Mau.
Kenta ameonyesha wasiwasi wake kwamba watu bado wameanza tena kuvamia eneo la vyanzo vya maji akimtaka Waziri huyo kuchukua hatua kali kwa watu binafsi ambao wana nia ya kuharibu msitu.
Wakati uo huo, mbunge huyo wa zamani amemsuta Gavana wa eneo hilo Patrick Ntutu kwa madai ya kutokuwa mwaminifu katika dhamira yake ya kulinda na kuhifadhi Hifadhi ya Maasai Mara.
Kenta anasema Hifadhi hiyo ni ya Jumuiya ya Wamasai na kwa hivyo jaribio lolote la kuhamisha umiliki wake kwa mtu binafsi au shirika linapaswa kupingwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo amesema wakazi wa eneo hilo wanapaswa kupewa muda wa kushiriki katika suala la mpango wa usimamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara na michango yao kujumuishwa.
Aidha vile vile amemshutumu Gavana Ntutu kwa madai ya kuharakisha mchakato huo na kudai inaonekana kuna mambo kadhaa ambayo hayaeleweki katika nyaraka za mpango huo ambayo yanafaa kujadiliwa zaidi.
Kadhalika serikali ya kitaifa Kenya ilifichua kuwa inafahamu madai ya ufujaji wa pesa za zaidi ya shilingi. milioni mia 910 na serikali ya kaunti ya Narok na kuitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC kuingilia kati na kuchunguza suala hilo.