‘Nisaidie Nirudishiwe Pesa Zangu!’ Sonko Amsihi Rais Ruto
Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko amemwomba Rais William Ruto amsaidie kurejesha pesa zake ambazo zilizuiliwa na mahakama.
Wakati wa uzinduzi wa Tume ya Mito ya Nairobi Sonko alisema kuwa uongozi wa Ruto umekuwa afueni kwa wale ambao walishtakiwa wakati wa utawala wa Uhuru.
Aliomba Rais aingilie kati ili kumuondoa kwenye ndoano, akidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) inataka kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama wa kumuondolea mashtaka ya rushwa na utakatishaji fedha.
Sonko alitoa wito wa usawa, akisema kwamba pesa zake zinafaa kurejeshwa kwake, sawa na naibu wa rais Rigathi Gachagua.
Mnamo 2020, Mahakama Kuu ilizuia takriban Ksh 18 milioni katika akaunti 10 za benki za gavana huyo wa zamani wa Nairobi.
Vile vile, mnamo 2022, Mahakama Kuu iliamuru kwamba Ksh.202 milioni kutoka kwa akaunti ya benki ya Gachagua zichukuliwe kwa serikali, kwa msingi kuwa zilikuwa mapato ya ufisadi.
Hata hivyo, mnamo Februari 1, 2023, Wakala wa Kurejesha Mali (ARA) ulimrudishia Gachagua pesa hizo, akisema alieleza chanzo na uhalali wa pesa hizo kuridhisha.