Kituo Cha 2 Cha JKIA Kufungwa Kwa Siku 2
Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (KCAA) imeagiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kufunga Terminal 2 Ijumaa, Februari 24 na Jumapili, Februari 26.
KCAA imesema kuwa kufungwa kutasaidia vikosi vya usalama katika kuwezesha harakati za Mke wa Rais wa Marekani, Jill Biden.
Kituo cha 2 kitafungwa kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa 5 jioni siku ya Ijumaa, Februari 24, na kuanzia saa 6 asubuhi hadi saa 6 jioni Jumapili, Februari 26.
Jill Biden ameratibiwa kukutana na mwenzake wa Kenya Rachel Ruto, pamoja na maafisa wengine wakuu serikalini, wakiwa nchini.
Hii ni ziara ya kwanza ya Jill Biden nchini Kenya kama Mke wa Rais wa Marekani na ziara yake ya tatu nchini Kenya kwa ujumla.
Wakati akitangaza ziara ya Mke wa Rais wa Marekani nchini Kenya, Ubalozi wa Marekani ulisema kuwa ziara ya Jill ilikuwa ni kuimarisha ushirikiano wa Marekani katika Bara la Afrika na kuendeleza vipaumbele vya pamoja katika kanda hiyo.
Zaidi ya hayo, atajadili masuala ya uwezeshaji wa vijana na hatua za kukabiliana na ukame ambazo zinafaa kutekelezwa kote nchini.
Kulingana na ripoti kutoka kwa vyomba vya habari, ziara ya Mke wa Rais inajiri kabla ya ziara zinazotarajiwa za mumewe Rais Joe Biden na maafisa wengine wakuu wa utawala baadaye mwaka huu.
Aidha Biden pia atatembelea Namibia wakati wa safari yake barani Afrika ambapo anatarajiwa kuelekeza mijadala yake juu ya kuimarisha sera za vijana na utamaduni wa ujasiriamali.
Viongozi wengine wa Marekani waliozuru nchini hivi majuzi ni pamoja na Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield na Waziri wa Hazina wa Marekani Janet Yellen waliozuru nchini Januari 2023.
Kando na kukutana na wajasiriamali wa Kenya wakati wa ziara yake, Greenfield ilishirikiana na maafisa wa Umoja wa Mataifa, wanafunzi wa uhusiano wa kimataifa, na wanafunzi wa zamani wa programu za kubadilishana za Marekani.