Home » DPP Kuamua Hatima Ya Washukiwa 10 Wa Kashfa Ya Dhahabu Ya Ksh.67M

DPP Kuamua Hatima Ya Washukiwa 10 Wa Kashfa Ya Dhahabu Ya Ksh.67M

Hatima ya washukiwa 10 wanaohusishwa na sakata ya dhahabu ya Ksh.67 milioni sasa iko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

 

Hii ni baada ya washukiwa hao kufika mahakamani jana Jumatatu na kutojibu mashtaka kwa sababu faili ya polisi imetumwa kwa afisi ya DPP kukaguliwa kabla ya kufanya uamuzi wa kuwafungulia mashtaka au la.

 

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Esther Kimilu aliagiza kesi hiyo kutajwa Machi 6, ili DPP athibitishe njia ya kuendelea na kesi hiyo.
Hakimu pia aliwaongezea washukiwa dhamana ya pesa taslimu mapema ya Ksh.100,000 kila mmoja akisubiri maelekezo zaidi.
Washukiwa hao ni pamoja na Wakenya wanane, mmoja Mgiriki na mmoja raia wa India.

 

Miongoni mwao ni Samuel Wathika Gathuru anayetambuliwa kuwa afisa wa polisi, Moses Otieno Oketch, Patroba Odhiambo Tobias, Elisha Mbadi Kimbero, Teddy Samora Kowino, Loaennis Kaisarios, Mugabe Patrick Biriko, Seth Steve Okute, Bruno Otieno Oliende na Collins Kiprotich Lang’at.

 

Kulingana na stakabadhi za mahakama, Okute ni kiongozi wa kisiasa ambaye aliwania kiti cha ubunge cha Karachuonyo 2022 kwa tiketi ya chama cha ODM, huku Oliende akiwania kiti cha Ubunge wa Suna Mashariki katika Kaunti ya Migori akiwa mgombea Huru.

 

Okute na Oliende walishtakiwa tofauti kwa kupatikana na Marjorie Grant USD 100,000 sawa na pesa za Kenya (Ksh.12.7 milioni) kwa kudanganya kuwa kampuni ya Newsky ya Global cargo Movers Intern Ltd ilikuwa na uwezo wa kulipa ushuru wa kilo 33 za dhahabu iliyosafirishwa kutoka Burkina Faso.

 

Wawili hao walinaswa kufuatia ripoti iliyotolewa na mwathiriwa, ambaye ametambuliwa kama Bi Marjorie Grant, mwekezaji wa Marekani anayeishi Los Angeles, California.

 

Maafisa wa upelelezi wanasemekana kuokota Bastola aina ya Baretta iliyokuwa na risasi 13 kutoka Okute.

 

Wakiwa nyumbani kwa Otieno huko Kitusuru, Kaunti ya Nairobi, wahudumu hao walipata masanduku ya chuma nzito, yanayoshukiwa kutumiwa kuhifadhi habari muhimu ambazo kwa sasa zinawasaidia maafisa hao katika uchunguzi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!