Mfalme Zumaridi Atoka Gerezani Baada Ya Kukaa Mwaka Mmoja

Mfalme Zumaridi ni miongoni mwa wahubiri wa dini maarufu nchini Tanzania. Ndani na nje ya jiji la Mwanza kwa miaka kadhaa, Zumaridi ambaye pia hujiita mungu wa duniani, amekuwa akitoa huduma ya maombezi, mahubiri na hata tiba kwa magonjwa kadhaa anayodai kuwa na uwezo wa kuyaponya.
Mnamo Februari 18, amehitimisha kifungo chake cha mwaka mmoja katika Gereza la Butimba jijini Mwanza nchini Tanzania na kurejea nyumbani kwake huku akipokelewa na mamia ya waumini wake.
Zumaridi alikutwa na hatia ya kuzuia maofisa wa Umma kutekeleza majukumu yao katika kesi ya jinai namba 10/2022, alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekobora. Baada ya kutiwa hatiani alitumikia mwezi mmoja kutokana na kukaa rumande miezi 11 ambapo leo Februari 18, 2023 amehitimisha kifungo hicho na kujumuika na waumini wake.
Baada ya kuwasili nyumbani kwake, Zumaridi amepokewa na ndugu na mamia ya waumini wake huku wakiimba na kucheza muziki, wengine wakimsujudia huku wengine wakipeperusha vitambaa vyeupe.
Baada ya kufika nyumbani kwake, huku akiwa amesimama juu ya gari lake, Zumaridi aliteremka huku akiwa amezungukwa na walinzi wake “Mitume” waliovaa sare za pinki (mashati) na (suruali na sketi) nyeusi.
Baada ya kupokelewa Zumaridi amepanda madhabahuni na kuanza kuhutubia waumini hao huku akiwashukuru kwa kumuombea wakati wote wa kesi iliyokuwa inawakabili.