Jalang’o Aondoka Katika Mkutano Wa Azimio Machakos
Mbunge wa Lang’ata Felix Odiwuor Jalang’o amefukuzwa nje ya mkutano wa wabunge wa Azimio la Umoja unaoendelea Maanzoni Lodge kaunti ya Machakos.
Vurugu zimeshuhudiwa katika kituo hicho baada ya kundi la wanaume kumzuia Jalang’o kuingia katika jumba la mikutano.
Baada ya purukushani hiyo fupi, mbunge huyo aliruhusiwa kuingia ndani, lakini dakika chache baadaye akatolewa.
Akizungumza na wanahabari baada ya kutimuliwa, Jalang’o amedai kuwa mwanachama wa usalama wa Raila Odinga alimtaka atoke nje ya ukumbi huo.
Matatizo hayo ya wabunge yamehusishwa na mkutano aliofanya na Rais William Ruto siku ya Jumatatu.
Alipoulizwa iwapo ataomba radhi kwa kuchukua mwelekeo tofauti na chama chake, Jalang’o alisema; “Hakuna msamaha kuhusu hilo, nilikwenda huko kwa maendeleo.”
Mbunge huyo wa Lang’ata alizuru Ikulu Jumatatu akiwa na wabunge wengine wakiwemo; Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki, Independent), Paul Abuor (Rongo), John Owino (Awendo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda .