Polisi Wana Haki Ya Kuchunguza Kila Mwanasiasa Asema Khalwalwe
Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amesema kuwa operesheni ya usalama iliyoendeshwa katika makazi ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i jana Jumatano usiku haikuwa na makosa kwa vyovyote vile.
Kulingana na Seneta Khalwale, hakuna yeyote, wakiwemo wale ambao wamekashifu operesheni hiyo, wanaojua sababu ya kweli iliyowafanya maafisa wa polisi kuzingira nyumba ya Matiang’i, na huenda hata anachunguzwa.
Akizungumza kwenye kipindi cha runinga humu nchini, mwanasiasa huyo mkongwe ameteta kuwa ikiwa kweli Matiang’i alikuwa anachunguzwa, polisi walikuwa na haki ya kisheria ya kuzuru eneo hilo usiku na wangefanya hivyo ili kumkamata.
Khalwale ameongeza kuwa wanachama wa tabaka la kisiasa wanapaswa kuacha kubahatisha kuhusu suala hilo hadi ripoti rasmi ya kwa nini operesheni hiyo ilifanywa itolewe.
Ametaja maoni yaliyotolewa na kiongozi wa (ODM) Raila Odinga ambaye alitaja operesheni hiyo kuwa “haikubaliki kabisa”, akisema kuwa alizungumza bila kwanza kufahamu sababu za ujio huo wa polisi.
Kulingana na ripoti, idadi isiyojulikana ya maafisa wa polisi mashuhuri walionekana nyumbani kwa Matiang’i Karen usiku.
Sababu ya operesheni hiyo ya usalama usiku haikuweza kufahamika mara moja, huku kukiwa na ripoti kwamba timu ya usalama iliripotiwa kuondoka mara tu baada ya vyombo vya habari kutangaza habari za operesheni hiyo.
Wanasiasa wengi kutoka muungano wa Azimio la Umoja walimiminika katika jumba hilo muda mfupi baada ya habari kuibuka wakiongozwa na Raila ambaye alikashifu vikali oparesheni hiyo, akiitaka serikali kuhusika na tukio hilo, akiapa kusimama na Dkt Matiang’i.