Home » Azimio Kufanya Mkutano Na Wabunge Wake Hii Leo

Muungano wa Azimio La Umoja One-Kenya umepanga mkutano wake hii leo wa kundi la wabunge ili kuziba nyufa ndani ya muungano huo ambao umeshuhudia viongozi kadhaa kutoka kwa mrengo huo wakijiunga na Muungano wa Kenya Kwanza.

 

Maelezo kuhusu mkutano huo yamesalia kuwa machache lakini mojawapo ya ajenda kuu itakuwa kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama kutoka Jubilee na ODM ambao wamekaidi ajenda ya muungano huo.

 

Mkutano huo unalenga kupendekeza njia ya kusonga mbele kufuatia kuondolewa kwa wabunge kadhaa na pia kusitisha hatua kama hiyo ambayo inaweza kutatiza harakati za kisiasa za kiongozi wake Raila Odinga.

 

Hivi majuzi, Rais William Ruto amevamia kambi ya kisiasa ya Odinga kwa kuwanyakua viongozi waliochaguliwa na wasiochaguliwa kutoka kwa vyama tanzu.

 

Takriban wabunge 32 wa Jubilee wamevunja safu na Azimio La Umoja One-Kenya na kuungana na Rais William Ruto wa Kenya Kwanza .
Rais william ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua walikuwa na mkutano na wabunge wanaotoka katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Wakiongozwa na Mbunge Mteule Sabina Chege na Mbunge wa EALA Kanini Kega viongozi hao walijitolea kufanya kazi na serikali wakitelekeza ajenda ya mapinduzi na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Mbunge wa Eldas Adan Keynan alisisitiza kwamba wataungana ili kuimarisha ajenda ya utawala wa Rais Ruto.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wabunge David Kiaraho (Ol Kalou), Irene Njoki (Bahati), Zachary Kwenya (Kinangop) na Shadrack Mwiti (Imenti Kusini) Mark Mwenje (Embakasi Magharibi), Amos Mwago (Starehe), Dan Karitho (Igembe ya Kati), Stanley Muthama (Lamu Magharibi) na Joseph Githuku (Lamu)

 

Jubilee ni sehemu ya Muungano mkubwa wa Azimio la Umoja One-Kenya ulioshindana na Muungano wa Ruto wa Kenya Kwanza katika uchaguzi wa Agosti 2022.

 

Haya yanajiri saa 24 tu baada ya viongozi tisa wa ODM kufanya mkutano na rais William ruto kwa makusudi ya maendeleo katika maeneo bunge yao.

 

Mvutano wa kisiasa ndani ya muungano wa Azimio La Umoja One-Kenya umeendelea kukumba vuguvugu la kisiasa la Odinga.

 

Ingawa hawajajiunga rasmi na Muungano wa Kenya Kwanza, viongozi hao huenda wakaendelea kususia harakati za Odinga nchini kote na kuzingatia ajenda ya serikali.

 

Hili ni pigo la kisiasa kwa Odinga kwani Rais Ruto amefaulu kuwanyakua viongozi hao kutoka uwanja wake wa jadi wa kisiasa huko Nyanza.
Miongoni mwa viongozi ambao wamehudhuria mkutano huo ni pamoja na Tom Ojienda (Kisumu), Shakeel Shabir (Kisumu Town Mashariki) na Caroli Omondi (Suba Kusini).

 

Wengine ni pamoja na Elisha Odhiambo (Gem), Gideon Ochanda (Bondo), Phelix Odiwour AKA Jalango (Langata) na Mark Nyamita (Uriri).
Haya yanajiri kufuatia mkutano wa kisiasa wa Kibra wikendi ambapo baadhi ya washirika wakuu ndani ya kambi ya Odinga walikosekana.

 

Hali inayozua taharuki kuhusu iwapo muungano huo utasalia sawa huku majaribio ya Rais Ruto ya kuwashawishi viongozi kote nchini katika harakati zake za kuleta umoja yakiendelea.

 

Viongozi ambao wameshindwa kuhudhuria mikutano mitatu iliyoandaliwa na Odinga kufikia sasa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Azimio Junet Mohammed, Mwenyekiti wa ODM John Mbadi, Makamu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Joho.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!