Raila Adai IEBC Ilitumia Sava Za Kigeni

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga sasa anasema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitumia sava ya kigeni kuwasilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9 mwaka jana.
Raila ameyasema hayo wakati wa mkutano na viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya katika Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga.
Mkutano huo ulikuwa wa kupanga mkutano katika Viwanja vya Jacaranda Jumapili ijayo.
Katika ufichuzi wake, kiongozi huyo wa upinzani ameeleza kuwa uchunguzi wa timu yake ulifichua kuwa IEBC ilikuwa na sava nne; mbili nchini na mbili nje ya nchi.
Hata hivyo, Raila anasema kuwa ni moja tu kati ya sava hizo nne iliyotumika kuwasilisha matokeo, ikidaiwa kutuma matokeo kutoka nchini Venezuela.
Raila pia anasema moja ya sava hizo ilikuwa nchini Uholanzi na mbili zilizokuwa Kenya zilikuwa zimewekwa katika jumba la Anniversary Towers na Industrial Area.