Mbunge Koech Apuuzilia Mbali Madai Ya Raila
Mbunge wa Belgut katika kaunti ya kericho Nelson Koech amepuuzilia mbali madai yaliyotolewa na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga kwamba Uchaguzi Mkuu wa 2022 ulimpendelea Rais William Ruto.
Kulingana na Mbunge Koech, Raila anapenda kuwakusanya wafuasi wake ili kupinga serikali tawala kila anaposhindwa katika uchaguzi na hii pia haina tofauti.
Kwenye mahojiano na Runinga moja humu nchini, Mbunge Koech amedai kuwa anachokusudia Raila ni kulazimisha serikali ili kujinufaisha kisiasa, akimshtumu kama mtu ambaye ana kiu cha mamlaka.
Koech amebainisha kuwa Raila, wakati wa mkutano wake wa hadhara jana Jumatatu, alifaa kutangaza mageuzi ambayo yanafaa kupitishwa na serikali lakini badala yake akachagua mwelekeo tofauti.
Kuhusiana na matakwa ya Raila kwamba sava za uchaguzi zinapaswa kufunguliwa, Mbunge Koech amelitaja kuwa jambo la kawaida kwani Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa imehakikisha kuwa kuna uwazi wa kutosha katika uwasilishaji wa matokeo wakati wa upigaji kura.
Hayo yaliungwa mkono na Rais Ruto Jana aliposema kuwa IEBC iliendesha uchaguzi wa wazi na alifurahia mamlaka kamili kutoka kwa wananchi wa Kenya.