Home » Huenda Tom Osinde Aliuawa Nyumbani Kwake Nakuru

Sasa inaibuka kuwa marehemu afisa wa zamani wa Hazina Tom Osinde alipewa dawa za kulevya na kuuawa nyumbani kwake Nakuru kabla ya mwili wake kupelekwa Migori na kutupwa mto Kuja.

 

Haya ni kwa mujibu wa chanzo cha polisi kilicho karibu na uchunguzi huo ambao walizungumza na wanahabari lakini wakataka kutotajwa jina kutokana na unyeti wa kesi hiyo.

 

Chanzo hicho kilidai kuwa marehemu aliuawa siku hiyo hiyo ambayo alitangazwa kutoweka – Juni 18, 2023.

 

Mwili huo pia uliripotiwa kupatikana ukielea kwenye Mto Kuja mnamo Juni 22 – siku tano baada ya kutangazwa kutoweka – na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Migori Level Four ambako uliwekwa kama ‘John Doe’ kwani haukujulikani wakati huo.

 

Ni Jumatano usiku ambapo mwanafamilia, akiwa na afisa wa polisi, walienda hospitalini na kutambua vyema mwili huo kuwa wa Osinde.

 

Chanzo cha polisi kiliongeza kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha yanayoonekana kama yale yaliyopatikana kutoka kwa kitu butu, na kwamba gari la marehemu ambalo lilipatikana Jumamosi – pia lilikuwa na chembe za damu ndani.

 

Mwili wa Osinde Alhamisi ulihamishwa kutoka kituo cha Migori hadi katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kisii Level Five ambapo uchunguzi wa maiti utafanywa.

 

Watu wawili tangu wakati huo wamekamatwa kuhusiana na kifo cha afisa wa zamani wa Hazina, na kwa sasa wanasaidia polisi kufanya uchunguzi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!