Home » Wabunge Washinikiza Uchunguzi Wa Umma Kuhusu Kashfa Ya NHIF

Wabunge Washinikiza Uchunguzi Wa Umma Kuhusu Kashfa Ya NHIF

Uchunguzi wa umma kuhusu udanganyifu wa matibabu unaohusisha Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) utazinduliwa hivi karibuni.
Kamati ya Bunge ya Afya imetoa tangazo hilo baada ya mkutano na wasimamizi wakuu.

 

Hii inafuatia kufichuliwa kwa baadhi ya hospitali za kibinafsi zilivyokuwa zikishirikiana na wafanyikazi wasio waaminifu wa NHIF kulaghai mamilioni ya pesa kupitia madai ya uwongo.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mbunge wa Endebess Robert Pukose amesema uchunguzi wa kina pekee ndio utakaofichua ukweli wa ulaghai huo mkubwa na kuongeza kuwa ni wakati wa mabadiliko makubwa kufanywa katika bima ya afya.

 

Sehemu ya uchunguzi utazingatia madai ya upendeleo unaotekelezwa na hospitali zinazomilikiwa na watu binafsi kuliko taasisi za afya za umma.

 

Mbunge wa Moyale Prof. Guyo Waqo Jaldesa ambaye ni sehemu ya kamati ya wanachama 15 anasema bado haieleweki jinsi hospitali ya kibinafsi inaweza kufanya upasuaji zaidi kuliko hospitali maarufu za umma kama vile Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) na Hospitali ya Kufundisha na Rufaa ya Moi (MTRH) .

 

Akiunga mkono pendekezo la uchunguzi wa umma, Mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek amejutia vitendo vya ulaghai vinavyoendelea katika hazina ya bima.

 

Maoni yake yameungwa mkono na Mbunge wa Nyeri Mjini Dancun Mathenge ambaye amesema ni uchunguzi wa umma pekee utakaofichua uozo huo katika NHIF.

 

Baraza la Madaktari wa Meno nchini (KMPDC) tayari limesimamisha vituo vyote vinane vya matibabu vilivyohusishwa na kashfa hiyo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!