Mali Yaharibiwa Wanafunzi Wa Chuo Kikuu Mombasa Wakiandamana

Sehemu ya Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa(TUM) imeteketea kwa moto hii leo Jumatatu saa sita mchana huku wanafunzi wakiandamana kupinga utawala.
Wingu la moshi lilionekana kutoka chuo hicho chenye makao yake mjini Mombasa katika video zilizosambazwa mtandaoni, wanafunzi walipoandamana kuzunguka chuo hicho wakiwa wamebeba mabango na vijiti.
Moto mkubwa ulionekana ukiharibu vibanda katika kituo cha wanafunzi wa chuo kikuu.
Wanafunzi hao walitaka maelezo kutoka kwa uongozi juu ya nyongeza ya karo na kile walichokitaja kuwa ni kufutiwa usajili wa wanafunzi kwenye tovuti ya mtandao kutokana na kukosa alama.
Walishutumu sehemu ya kitivo cha uzembe.
Polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kwa wanafunzi hao ili kudhibiti hali.
Thamani ya mali iliyoharibiwa katika maandamano hayo haikuweza kufahamika mara moja.