Home » Familia Ya Mwanafunzi Aliyeuwawa Na Al-Shabaab Yadai Haki Itendeke

Familia Ya Mwanafunzi Aliyeuwawa Na Al-Shabaab Yadai Haki Itendeke

Jua linapochomoza asubuhi tulivu katika Kijiji cha Salama, Mama Pamela Agutu yuko katika majonzi.

 

Watu watano waliuawa katika shambulizi mwishoni mwa juma, akiwemo mjukuu wake Barrack Hussein, mwanafunzi wa kidato cha 3 katika Shule ya Sekondari ya Bakanja.

 

Pamela anadai kuwa zaidi ya wanaume 40 waliovalia mavazi ya kijeshi walifika nyumbani kwao na kuwaambia walale kabla ya kuchoma moto mahali hapo na kumshambulia mwanafunzi mwenye umri wa miaka 19 ambaye alikuwa akizuru kwa mapumziko ya katikati ya muhula.

 

Baadaye, washambuliaji waliwaua wanaume wengine wanne, akiwemo mzee wa miaka 60 ambaye walikuwa wamemfunga kabla ya kumuua.
Pia walichukua vyakula, kutia ndani sukari, maharagwe na kuku, wakachinja hapo hapo kabla ya kuondoka.

 

”Walichoma nyumba yetu na kumpiga risasi ya tumbo kabla ya kumchinja…ninahofia maisha yangu na ya watoto wangu wengine…” Alisema.
Shambulio hilo ambalo linaaminika kutekelezwa na wanamgambo wa Al-Shabaab, limeacha jamii katika mshangao na huzuni.

 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Rhoda Onyancha alitembelea eneo la tukio na kuahidi kuwa ulinzi utaimarishwa, na wahusika wa kitendo hicho cha kinyama watafikishwa mahakamani.

 

Uchunguzi bado unaendelea ili kubaini chanzo cha shambulio hilo.

 

”Uchunguzi unaendelea natoa wito kwa wakazi wa salama kuwa waangalifu tutawashughulikia wahalifu hawa bila huruma.” Alisema Reginal Boss.

 

Wakati uo huo, Pamela anatatizika kukubaliana na kufiwa na mjukuu wake, ambaye anamtaja kuwa mwanafunzi mzuri na mwenye matumaini. Anasema kwamba Barrack alikuwa na ndoto ya kuwa daktari na alikuwa akifanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yake.

 

Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama, ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuharakisha mchakato wa uchunguzi na kuwaweka wahusika mahakamani. Pia ameitaka serikali kuboresha mfumo wa mitandao katika eneo hilo kwa mawasiliano na mwitikio bora wa vyombo vya ulinzi na usalama.

 

”Naviomba Vyombo vya Usalama viharakishe uchunguzi wao na kuhakikisha tunafika mwisho wa jambo hili hatuwezi kuruhusu watu kuuawa kila siku lazima kitu kifanyike inatosha.” Alisema mbunge huyo.

 

Huku jamii ikiomboleza kuondokewa na wapendwa wao na kujaribu kukubaliana na ukatili huo usio na maana, wamebaki wakiwa na matumaini kwamba haki itatendeka na wataweza kuishi bila hofu ya kushambuliwa zaidi.

 

Kwa Mama Pamela na familia nyingine zilizopoteza wapendwa wao, maisha hayatakuwa sawa tena.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!