Waziri Chelugui: Nyeri Yaongoza Katika Urejeshaji Wa Mkopo Wa Hustler Fund
Nyeri inaongoza katika orodha ya kaunti zilizo na urejeshaji wa juu wa mkopo, miezi mitano baada ya Hustler Fund kuzinduliwa.
Kulingana na data ya hivi punde iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mawaziri la Maendeleo la MSME Simon Chelugui, Nyeri inaongoza kwa asilimia 76.3 ikifuatiwa na Kiambu kwa asilimia 75.3 huku Nyandarua ikichukua nafasi ya tatu kwa asilimia 74.5.
Nairobi, ambayo inajivunia kuwa na idadi kubwa zaidi ya watumiaji milioni 2, iko katika nafasi ya nne kwa kiwango cha urejeshaji cha asilimia 73.8.
Kaunti zingine katika kumi bora ni pamoja na Laikipia (73.6%), Nandi (73.5%), Murang’a (73.3%), Embu (73.1%), Uasin Gishu (73.1%) na Nakuru (72.9%).
Kitaifa, kiwango cha ulipaji kinafikia asilimia 69, huku Chelugui akisema: “Tunaunda HISTORIA sana inayoungwa mkono na data. Nimefurahishwa sana na mtazamo chanya ulioonyeshwa na walengwa wengi na Wakenya kwa jumla.”
Kwa upande wa umri, vijana wanaoangukia kati ya miaka 18-29 wanaongoza kwenye chati ya wakopaji kwa asilimia 38.5 wakifuata wale kati ya 30-39 ambao wanadhibiti asilimia 28.8. Watu wenye umri kati ya asilimia 40-49 hadi sasa wameandikisha asilimia 17.5 ya kiwango cha kukopa.
Kwa upande wa jinsia, wanaume wengi wanakopa Hustler Fund ikilinganishwa na wanawake kwa asilimia 66 na asilimia 34 mtawalia.
Chelugui aliongeza kuwa, kufikia sasa, Ksh.31.5 bilioni zimetolewa huku urejeshaji wa mkopo ukifikia Ksh.21.2 bilioni.
Aidha Akaunti ya akiba sasa inafikia Ksh.1.5 bilioni.
Idadi ya watu ambao wamejiandikisha na mfuko huo sasa inafikia milioni 20 huku milioni 7.1 wamekopa kutoka kwa kitita na kurejesha zaidi ya mara moja.
Waziri huyo ameendelea kusema kuwa wakati Wakenya wengi zaidi wanatumia mulika mwizi (asilimia 55) kuliko simu janja (asilimia 45) katika bidhaa ya kibinafsi, simu janja hugeuza meza inapofikia bidhaa ya vikundi ambayo ilizinduliwa hivi majuzi.
Chelugui aliongeza kuwa, kufikia sasa, jumla ya vikundi 170, 376 vimezinduliwa na takriban Ksh.20 milioni zimetolewa.
Nairobi inaongoza katika orodha ya kaunti zilizo na vikundi vilivyosajiliwa zaidi, 10, 957 ikifuatiwa na Trans Nzoia ambayo inajivunia vikundi 9,792. Meru imesimama kwenye nambari tatu ikiwa na vikundi 9, 647.
Kaunti zingine katika kumi bora ni pamoja na: Nakuru, Kiambu, Bomet, Nandi, Uasin Gishu, Narok na Kisii.