Spika Wa Bunge La Meru Atetea Hospitali Iliyotajwa Kwenye Sakata Ya Wizi Wa NHIF
Maswali yameibuka kuhusu uongozi wa Bunge la Kaunti ya Meru uliogawanyika kuhusu uchunguzi unaoendelea kuhusu sakata ya bima ya kitaifa ya matibabu ya NHIF.
Mnamo Jumatano, spika wa Bunge la Kaunti ya Meru Ayub Bundi alitetea Hospitali ya Jekim, ambayo ni mojawapo ya vituo vinavyohusishwa na kashfa hiyo.
Hii ni licha ya kamati ya afya kutokamilisha uchunguzi wake.
Spika Bundi alidai kuwa kulingana na uchunguzi wa bunge, hospitali za Jekim hazikuhusika katika kashfa ya NHIF.
Alisema kituo hicho kilifanya uchunguzi wa x-ray pekee ambao walilipwa elfu moja kila mmoja na hawakupokea hata shilingi moja kutoka NHIF kwa sababu wagonjwa hawakutibiwa katika kituo hicho.
Bundi alisema ni kinyume cha sheria kwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha kufunga hospitali za Jekim kwa kuwa hospitali hiyo haikuhusika katika sakata hiyo.
Mnamo Alhamisi, mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la kaunti ya Meru Douglas Mutea alisema uchunguzi kuhusu sakata ya NHIF bado unaendelea na ripoti kamili itatolewa ndani ya wiki tatu.
Mutea alipinga taarifa za spika kwamba walimwita mmiliki wa Hospitali ya Jekim mwezi mmoja uliopita, na kuongeza kuwa Kamati imepanga kumwita Jumatano wiki ijayo.