Ombi Lawasilishwa Kutaka Kumtimua Gavana Wa Isiolo

Kesi imewasilishwa katika Mahakama Kuu ikitaka Gavana wa Isiolo Abdi Guyo na naibu wake John Lowasa kuondolewa afisini kwa kuhamia chama cha United Democratic Alliance (UDA) kutoka chama cha Jubilee.
stakabadhi zilizowasilishwa na wapiga kura wanne ambao ni Guyo Ali, Mohammed Wario, Teddy Muturi na Steven Kihonge zinadai kuwa Gavana Guyo na Lowasa wamejiondoa kutoka kwa chama cha Jubilee na kusajiliwa rasmi kuwa wanachama wa UDA na kwa hivyo wanapaswa kuzuiwa kufanya shughuli zozote katika serikali ya kaunti kwani hatua hiyo ina maana moja kwa moja wamepoteza viti vyao.
Kupitia wakili Kibe Mungai, wapiga kura hao wanasema kujitoa kwa wawili hao kunadhoofisha na kutatiza demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya na haswa katika Kaunti ya Isiolo.
Guyo na Lowasa walishinda kiti cha ugavana kwa tikiti ya Jubilee Party lakini wakahamia chama cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto wiki jana.
Gavana Guyo na naibu wake walitangaza kujitoa kwa UDA mnamo Juni 2, 2023, na kusajiliwa hadharani kama wanachama wake wakati wa hafla ya umma iliyoongozwa na katibu mkuu wa chama hicho Cleophas Malala.
Sasa wanataka maagizo yatolewe kwa Msajili wa vyama vya kisiasa kuitaarifu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba Gavana Guyo na Lowasa wamekoma kuwa wanachama wa Jubilee, kwa mujibu wa Kifungu cha 34(1) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa.
Wapiga kura hao wanne pia wanataka mahakama itoe amri ya kukizuia chama cha UDA kuunga mkono kukiuka na kuasi viongozi waliochaguliwa wa Jubilee .
Kulingana na walalamishi, mahakama inapaswa kuchukua hatua haraka na kulinda katiba kwa kuhakikisha “njama ya UDA na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuhujumu demokrasia ya kikatiba na kurejesha udikteta wa kisiasa nchini Kenya haifaulu.”
Mungai pia anasema ombi hilo linaibua maswali makubwa ya sheria na haki za kisiasa, hivyo linapaswa kusikilizwa na kuamuliwa na Mahakama Kuu yenye majaji wasiopungua watano.