Shakahola: Wakaguzi Wa Ardhi Wasema Mackenzie Anamiliki Ekari 3716
Miili mingine mitano imefukuliwa na maafisa wa upelelezi wanaoendelea na awamu ya tatu ya zoezi hilo katika Msitu wa Shakahola kaunti ya kilifi na kufanya idadi ya watu waliofukuliwa kufikia 247.
Kufukuliwa kwa makaburi mengine 22 yaliyogunduliwa wiki jana kunalingana na ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki na mkuu wa idara ya upelelezi na makosa ya jinai DCI Mohamed Amin katika msitu wa Shakahola hii leo Jumanne.
Wakati wa zoezi hilo Jumanne, timu ya wapima ardhi kutoka Wizara ya Ardhi iliamua kwamba ardhi inayomilikiwa na mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie kwa hakika ni ekari 3716 na wala si ekari 800 kama ilivyoripotiwa awali.
Kulingana na waziri Kithure, eneo la uhalifu halitatumika tena kwa shughuli za binadamu, badala yake litageuzwa kuwa ukumbusho.
Wakati huo huo, wanajeshi wameweka kambi kwenye eneo hilo kubwa na wanatarajiwa kuanza kuunda barabara za muda baada ya kugawanya ardhi hiyo katika maeneo ya ekari 200 na 500 ili kurahisisha harakati huku msako wa makaburi zaidi ya watu wengi ukizidi.
Zaidi ya watu 242, wakiwemo watoto, wanasemekana kujiua kwa njaa katika kile kinachoitwa “mauaji ya Shakahola.”
Wapelelezi wanaochunguza tukio hilo la kushtua wanaamini waumini hao waliongozwa na mafundisho ya kidini kabla ya kuingizwa katika makazi ya muda ndani ya msitu wa Shakahola, ambapo walikufa kwa njaa.
Jumla ya sampuli 93 za DNA zimekusanywa, na watu 34 wanaohusishwa na tukio hilo wamekamatwa, akiwemo kiongozi wa madhehebu Paul Mackenzie.
Mahakama ya Mombasa mnamo Ijumaa iliagiza Mackenzie na washukiwa wengine 16 kusalia chini ya ulinzi wa polisi hadi Jumatano wiki ijayo ili kuruhusu kusikizwa kwa ombi la kutaka kuzuiliwa kwa siku 60 zaidi.