Home » Waititu Akosa Kufika Mahakamani

Ferdinand Waititu Picha kwa hisani

Kesi ambapo aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na wenzake 12 wanashtakiwa kwa tuzo isiyo ya kawaida ya zabuni ya barabara ya Ksh.588 milioni imeshindwa kuanza hii leo Jumatatu baada ya kukosa kufika mahakamani.

 

Mahakama imesikia kuwa mkuu huyo wa zamani wa kaunti aliugua na kuzimia nyumbani kwake jana Jumapili.

 

Wakili John Swaka alimweleza Hakimu Alex Kombo kwamba Waititu hangeweza kufika mahakamani kwa sababu amelazwa katika hospitali ya moja ya jiji.

 

Mahakama imeagiza kesi hiyo itajwe kesho Jumanne. Pia iliomba kukabidhiwa stakabadhi za matibabu za Waititu ili kuthibitisha ugonjwa huo.

 

Waititu alitimuliwa kama Gavana wa Kiambu mnamo Januari 2020.

 

Awali Mahakama Kuu ilikuwa imezuia mali 18 kuu na magari 7 ya Waititu kusubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

 

Maagizo hayo yaliyotolewa mwezi Juni na hakimu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Esther Maina yalimzuia Waititu, mkewe Susan Ndung’u na kampuni zao kuuza, kuhamisha au kuingilia kwa njia yoyote ile mali na magari hadi kesi hiyo itakapokamilika.

 

Waititu anadaiwa kujipatia kwa njia ya ulaghai mali ya thamani ya Ksh.1.94 bilioni kati ya 2015 na 2020 katika wadhifa wake kama gavana na mbunge wa zamani.

 

Aidha anashtakiwa kwa madai ya kufuja pesa za umma kwa kutoa zabuni za ununuzi kwa ulaghai kwa kampuni zilizotengwa kutoa huduma kwa Serikali ya Kaunti ya Kiambu.

 

Tume ya kupambana na ufisadi EACC inadai kwamba mara tu malipo ya kandarasi hizo potofu yalipofanywa na Kaunti ya Kiambu, kampuni zilizopewa kandarasi zingetuma pesa hizo kwa akaunti kadhaa za benki na biashara zilizosajiliwa chini ya jina la Waititu na la mke wake.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!