Ruto: Njugush, Butita Wanapata Pesa Nyingi Kuliko Mshahara Wangu
Rais William Ruto ameamuru kwamba ushuru uliopendekezwa kwa Content Creatores katika Mswada tata wa Fedha, 2023 utupiliwe mbali huku akiwasifu vijana wanaotumia nafasi ya mtandaoni kwa kufanya kazi nzuri na kuunda ajira.
Rais Ruto hasa amewataja Content Creators Timothy ‘Njugush’ Njuguna na Eddie Butita, ambao amewapongeza kwa kujituma na kuonyesha mfano mwema katika sekta hiyo.
Kulingana na rais, wabunifu hao wawili pamoja na wengine katika eneo moja wamepata mafanikio mtandaoni kwa hisani ya ushirikiano kati ya YouTube na serikali ya Kenya ambao umewawezesha kupata mapato ya kazi zao.
Kama matokeo, Rais ameendelea kusema kwamba Butita na Njugush wanaweza kuwa wanapata pesa nyingi kutokana na kazi yao mtandaoni kuliko maafisa wa serikali.
Hivyo ameiagiza Kamati ya Bunge ya Fedha na ile ya teknolojia na mawasiliano ICT kuangalia kwa mara ya pili kipengele cha kutoza ushuru Content Creators katika Mswada wa Fedha unaopendekezwa wa 2023 na kuilegeza kidogo ili vijana waendelee kujikimu kimaisha kupitia ufundi wao.
“Ninajua kuna pendekezo katika bajeti ya mwaka huu kuhusu maudhui ya kidijitali na waundaji… Nimeiambia kamati ya ICT na Fedha kulifanyia kazi. Wacha watoe nafasi zaidi, tuwaruhusu wajipange alafu baadaye si sisi wote tutalipa ushuru,” alisema Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi.
“YouTube imekuwa mshirika nasi, tulipowauliza waruhusu Wakenya kujisajili kutoka Kenya na kuchuma pesa, ulikuwa uamuzi mgumu lakini niseme asante sana kwa sababu wametusaidia … ndio maana tuna Njugush na Butita karibu. Hawa ndio wasanii wetu wazuri ambao leo wanachuma mapato kutoka kwa maudhui yao.
Rais Ruto aliongeza: “Pongezi sana waungwana, hao vijana wawili unaowaona wanaingiza pesa nyingi kuliko mshahara wangu, msiwaone hivi ati wamevaa sijui t-shirt, hao jamaa ni wajasiriamali makini, hongereni sana kwa kufuatilia kwa kuwa mfano kwa wenzetu wengi. vijana na kujua kwamba nafasi ya ubunifu, nafasi ya YouTube inapatikana kwa vijana wetu.”
Mswada wa Sheria ya Fedha, 2023 ulikuwa umependekeza, miongoni mwa maswala mengine mengi ambayo yalikosolewa vikali na umma, ushuru wa zuio wa 15% kwa mapato yanayotokana na maudhui ya kidijitali.
“Mtu anayetakiwa kukatwa kodi ya mali ya kidijitali ndani ya saa ishirini na nne baada ya kukatwa, atapeleka kwa Kamishna kiasi kilichokatwa pamoja na marejesho ya kiasi cha malipo, kiasi cha kodi kilichokatwa, na taarifa nyingine ambazo Kamishna anaweza kuhitaji,” ulipendekeza Mswada huo.