Mwanaume Auawa Baada Ya Mgodi Kuporomoka Huko Migori
Mwanaume mwenye umri wa miaka 31 amefariki baada ya ukuta wa mgodi kuporomoka katika eneo la uchimbaji mchanga katika kijiji cha Gwikonge, kaunti ndogo ya Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kuria Magharibi .Cleti Kimaiyo amesema marehemu aliyetambuliwa kama Daniel Wairimu Chacha mwenye umri wa miaka 31 alikuwa akichimba mchanga pamoja na kaka zake wawili John Chacha na Samwel Chacha wakati ukuta wa mgodi huo ulipoporomoka na vifusi hivyo kumwangukia.
Kimaiyo amesema Daniel Wairimu(marehemu) ambaye alitolewa kutoka kwa vifusi na ndugu hao wakishirikiana na wananchi alipata majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya Life Care kaunti ya Migori ambapo alithibitishwa kufariki alipokuwa akitibiwa.
Amesema mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kaunti ndogo ya Kuria Magharibi ikisubiri uchunguzi wa maiti na polisi.
Huku hayo yakijiri, kamanda wa polisi wa kaunti ndogo amewataka wachimbaji hao kuchukua tahadhari binafsi wanapofanya shughuli zao za uchimbaji ili kuepusha ajali hizo mbaya.
Kimaiyo amesema wachimbaji hao wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na zana sahihi za kujikinga wanapofanya shughuli zao za uchimbaji.