Pokot Magharibi: Visa Vya Wizi Wa Ng’ombe, Ujambazi Waongezeka
Uvamizi wa ng’ombe na mashambulizi ya kulipiza kisasi unaendelea licha ya kuwepo kwa Huduma ya Polisi ya Kenya na Jeshi la Ulinzi la Kenya ambao wanaendesha operesheni ya pamoja ya usalama katika eneo lenye matatizo ya usalama la bonde la Kerio pamoja na bone la ufa.
Katika kisa cha hivi punde zaidi, zaidi ya mifugo 150 wameripotiwa kuibwa kutoka eneo la Nasolot na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi kutoka kaunti ya Turkana.
Chifu wa lokesheni ya Nasolot Michael Mwotor alithibitisha kisa hicho akisema kuwa majambazi hao walitoroka kuelekea eneo la Kaakong kaunti ya Turkana.
Viongozi kutoka kaunti ya Pokot Magharibi wamekashifu kisa hicho wakiitaka serikali kurudisha mifugo iliyoibwa.
Viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong wametoa wito kwa timu ya usalama katika eneo hilo kuwa macho na tahadhari.
Lochakapong ametaja kuwa wako kwenye mazungumzo na wenzao katika kaunti ya Turkana ili kuhakikisha amani inarejea katika eneo hilo.
Mbunge huyo ameitaka serikali kurejesha amani na kukomesha wizi wa mifugo katika eneo hilo kwani watoto wao hawataenda shule kwa kuhofia mashambulizi ya kulipiza kisasi zaidi.
Seneta wa Pokot Magharibi Julius Murgor naye amesema kuwa timu ya usalama inafaa kukomesha ujambazi na wizi wa ng’ombe katika eneo hilo.
Kulingana naye ameshangaa kwa nini ujambazi na wizi wa ng’ombe bado unaendelea lakini operesheni ilikuwa inafanyika katika eneo hilo.
Aidha Kwa muda wa miezi miwili iliyopita, mamia ya mifugo iliibwa kutoka maeneo ya Ombolion, Sarimach, Cheprochpohog, Turkwel, Takaywa, Kases, Masol na Lami Nyeusi katika kaunti za Pokot Magharibi na Turkana zinazopakana na watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi.
Kamishna wa kaunti ya Pokot Magharibi Apollo Okello ambaye alizungumza wakati wa kusherehekea siku ya Madaraka katika uwanja wa Makutano alibainisha kuwa maafisa wa usalama wanapaswa kutambua maeneo ya kuweka kambi za usalama.
Haya yanajiri katikati ya mzozo wa mpaka kati ya viongozi wa Kaunti ya Pokot Magharibi na Turkana kuhusu hatua ya serikali kuweka kambi kuu ya usalama katika eneo la Porkoyo, karibu na eneo lenye utovu wa usalama la Lami Nyeusi.