Home » Mashirika Ya Kijamii Yamtaka Noordin Haji Kujiuzulu

Mashirika Ya Kijamii Yamtaka Noordin Haji Kujiuzulu

Baadhi ya mashirika ya kijamii yametoa wito kwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kujiuzulu kutokana na kile wanachodai kuwa utepetevu na utekelezaji duni wa majukumu yake.

 

Kulingana na mashirika hayo ya kijamii,Haji alishindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma,huku wakitaja visa kadha ambapo aliondolea mbali kesi za uhalifu na ufisadi dhidi ya baadhi ya maafisa wa umma.

 

Mashirika hayo pia yalipinga kupendekezwa kwa Haji kuhudumu kama mkurugenzi mkuu mpya wa shirika la ujasusi nchini.

 

Haya yanajiri siku mbili tu kabla ya Haji kukutana na Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni kwa ajili ya kuhakiki siku ya Jumanne wiki hii.

 

Mbali na hayo Baadhi ya viongozi kutoka Kaunti ya Garissa wamepuuzilia mbali mashirika ya kijamii ambayo yamejitokeza kukataa uteuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji na Rais Ruto kuongoza shirika la kijasusi wakisema kundi hilo lilikuwa na kisasi cha kibinafsi dhidi ya Haji.

 

Walimtetea Haji wakisema alifuata sheria alipotupilia mbali kesi za hali ya juu zilizohusisha maafisa wakuu serikalini.

 

Wakizungumza katika eneo bunge la Ijara wakati wa uzinduzi rasmi wa manispaa ya Masalani, viongozi hao waliahidi kuwakusanya wabunge wengine wenye nia moja ili kuhakikisha uteuzi wake unapitishwa bungeni.

 

Walisema kuteuliwa kwa Haji ni kielelezo tosha kuwa Rais ana imani naye na kwamba uadilifu wake hautiliwi shaka.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!