Mbunge Wa ODM Akashifu Mpango Wa Raila
Mbunge wa Lagdera Kaunti ya Garissa Abdikadir Hussein hii leo Jumamosi amekashifu mpango wa chama chake cha ODM wa kurejea maandamano akisema Wakenya hawana muda wa kufanya hivyo.
Kinara wa ODM Raila Odinga jana Ijumaa alisema kuwa muungano wa Azimio hautakuwa na chaguo ila kurejea katiaka maandamano iwapo kambi ya Kenya Kwanza itakosa kutii matakwa yao.
Haya yanajiri baada ya upande wa Azimio kusitisha mazungumzo ya pande mbili mnamo Jumanne ikitaja kutojitolea kwa wenzao wa Kenya Kwanza miongoni mwa sababu nyingine nyingi.
Akizungumza katika mji wa Masalani wakati wa uzinduzi wa manispaa ya Masalani, Hussein amesema licha ya kuwa yeye ni mbunge wa upinzani haungi mkono maandamano.
Kulingana na mbunge huyo, maandamano hayo yanasaidia tu kupunguza uchumi ambao tayari umeathirika.
Mbunge huyo ametumia fursa hiyo pia kupongeza mpango wa serikali ya Kenya Kwanza kumaliza uhaba wa maji unaoendelea katika eneo hilo.
Mchakato huo tayari unaendelea na ushirikishwaji wa wananchi ili kutambua wapi mabwawa yatajengwa.
Eneo bunge la Lagdera kwa muda mrefu limekumbwa na matatizo ya maji ikilinganishwa na maeneo mengine.
Hii imesababisha wakaazi hao kutembea umbali mrefu kutafuta bidhaa hiyo.
Katika baadhi ya matukio wale ambao huuza hufanya hivyo kwa ada kubwa.