Home » Polisi Wanasa Pombe Haramu Kapsabet

Polisi huko Kapsabet, Kaunti ya Nandi wamenasa pombe haramu iliyopakiwa kama chapa halisi za kampuni zilizoanzishwa zenye thamani ya Ksh600, 000 katika baa moja katika eneo la Kamobo.

 

Chifu wa mji wa Kapsabet Selina Too amesema vinywaji hivyo vilinaswa katika duka moja la mmoja wa wamiliki wa biashara eneo la Kamobo ambapo vilikuwa vikipakiwa ili kuuzwa katika baa zilizo karibu.

 

Too pia amesema maafisa wa usalama wanamsaka mmiliki wa baa iliyo nyuma ya kiwanda hicho haramu na wafanyikazi wake kadhaa ambao walitoroka polisi walipofika.

 

Vinywaji hivyo ghushi ambavyo usalama wake kwa watumiaji haukuweza kufahamika mara moja kwa mujibu wa chifu huyo, viliwekwa kwenye chupa zenye chapa ambayo ni maarufu kwa vijana.

 

Maafisa wa mamlaka ya ukusanyaji kodi nchini KRA pia wamethibitisha kuwa vinywaji vilivyonaswa vilikuwa na stempu ghushi zilizobandikwa walipopeleka vinywaji hivyo hadi Kaunti ya Kisumu ili kuthibitisha kwamba vinafaa kwa afya ya binadamu au la .

 

Afueni hiyo inajiri siku chache baada ya maafisa wa upelelezi kuanza uchunguzi katika kituo cha Kaptumo katika kaunti ndogo ya Aldai ambapo mvinyo na pombe kali ziliripotiwa kuongezeka.

 

Washukiwa hao pia wanasemekana kujihusisha na uchapishaji wa stempu ghushi za KRA zikiwemo zile za Uganda na Tanzania.

 

Operesheni hiyo inayoendelea inafuatia agizo la hivi majuzi la serikali lililowaagiza polisi kufanya operesheni kulenga bidhaa ghushi baada ya kufichua ushahidi wa kukwepa kulipa ushuru na “wafanyabiashara walaghai”.

 

Naibu Gavana wa Kaunti ya Nandi Yulita Cheruiyot ametoa wito kwa wakaazi kushirikiana bega kwa bega na maajenti wa usalama ili kukabiliana na tishio hilo.

 

“Vijana wengi wa siku hizi katika jamii zetu wanateseka kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, unaweza kufikiria kuwaingiza wakazi kwa dawa ambazo zinaweza kuharibu afya zao kweli, tunatarajia kizazi kijacho kiwe sawa ? La hasha, tafadhali polisi tukomeshe tabia hii katika kaunti yetu,” Yulita alisema.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!