Bei Ya Unga Wa Mahindi Kupanda Kwa Asilimia 10
Wakenya wanatarajiwa kupitia hali ngumu zaidi huku bei ya unga wa mahindi ikitarajiwa kupanda wakati serikali inapanga kuanzisha ushuru wa asilimia 10 kwa baadhi ya bidhaa.
Ushuru huo upo katika Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 ulio mbele ya Bunge.
Haya yanajiri wakati bei ya unga wa mahindi ikiwa juu na wakenya wengi wakitoa gadhabu zao kwa serikali iliyowaahidi mengi wakati wa kampeni.
Kwa sasa, mfuko wa kilo mbili wa Ndovu unauzwa Sh189, unga wa mahindi wa Jogoo unauzwa Sh208, unga wa mahindi wa Ajab Sh199, na unga wa mahindi wa Pembe unauzwa Sh 208.
Nyingine ni Soko Maize Meal, Sh207, na Raha Premium Kavagara, Sh262.
Zaidi ya hayo, mswada huo pia unapendekeza ushuru wa bidhaa wa Sh5 kwa kilo ya sukari, ambayo itasababisha bei ya juu.
Ikumbukwe, mfuko wa kilo mbili wa Kabras sasa unauzwa kwa zaidi ya Sh420, kumaanisha kwamba jamii za Kenya zitalazimika kuchimba zaidi mifukoni mwao ili kupata bidhaa hiyo.
Bei ya sukari imekuwa ikipanda nchini huku kukiwa na uzalishaji mdogo unaohusishwa na ukame wa muda mrefu ambao umekumba nchi huku Wakenya wakiendelea kukumbwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ongezeko la gharama ya juu ya maisha hakuna matumaini ya afueni kupatikana hivi karibuni .
Hatua hii inajiri baada ya serikali kutangaza kuongeza ada ya Hazina ya kitaifa ya Bima ya afya {NHIF} na Ile ya Hazina ya kitaifa ya Hifadhi ya Jamii {NSSF} .
Viwango vya sasa, ambapo wafanyakazi wanaolipwa hulipa kati ya Sh150 na Sh1,700 kulingana na malipo yao ya kila mwezi, vinaondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kiwango kisichobadilika cha asilimia 2.7 ya mshahara wao.
Vilevile kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha, kila mfanyakazi atalazimika kulipa asilimia tatu ya mshahara wake ili kuhudumia hazina mpya ya Maendeleo ya Makaazi.Serikali imesisitiza kuwa malipo hayo sio kodi bali ni akiba ingawa makato hayo yatalindwa na sheria na kutolewa kwa mishahara ya wafanyakazi .
Licha ya lalama za wafanyakazi wengi na waajiri kuhusu athari za tozo hiyo ,serikali inasisitiza kwamba mpango huo ni muhimu kwa sababu utaunda nafasi za ajira kwa mamilioni ya watu wasiokuwa na ajira nchini .
Hata hivyo kumekuwa na uhaba wa maelezo sahihi ya jinsi watu watakavyonufaika na miradi hiyo ya nyumba hasa ikizingatiwa kuwa wasiokuwa na kipato hawatochangia ilhali baadhi ya wanaolazimika kuchangia huenda wanalipa madeni ya ujenzi wa nyumba zao binafsi .