Home » Shakahola: Idadi Ya Waliofariki Yafika 241

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki ametangaza kwamba idadi ya waliofariki kule Shakahola kaunti ya Kilifi imeongezeka hadi 241.

 

Akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ufukuzi wa makaburi katika msitu wa Shakahola, waziri Kindiki amesema kwamba idadi hiyo imeongezeka baada ya mifupa mitano kupatikana na timu ya utafutaji na uokoaji, kufuatia kusitishwa kwa zoezi hilo Alhamisi, Mei 18 wiki jana.

 

Ameongeza kuwa mwathirika mwingine aliyeokolewa kutoka msituni alifariki dunia juzi jioni akiwa hospitalini baada ya kugoma kumeza chochote licha ya juhudi za wahudumu wa afya kumshawishi kula.

 

Wakati uo huo, watu 91 wameokolewa na waathiriwa 19 tayari wameunganishwa na familia zao.

 

Kulingana na Waziri Kindiki, makaburi zaidi yametambuliwa lakini yatachimbwa baada ya zoezi la uchunguzi wa miili hiyo 129 kukamilika.
Kindiki ameeleza haja ya kutoa nafasi katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi, ambako miili hiyo inahifadhiwa, ili kutoa nafasi kwa miili zaidi iliyofukuliwa.

 

Aidha, ameapa kuwa kazi ya utafutaji na uokoaji itaenezwa hadi maeneo jirani ya Tsavo na Galana Kulalu ambako anasema waathiriwa zaidi wanaaminika kutorokea.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!