Home » Raila Atoa Onyo Kali Kwa ORPP

Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga ametoa onyo kali dhidi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu kwa kile anachodai kushindwa kutekeleza mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa katika chama cha Jubilee.

 

Mkuu huyo wa Azimio amepinga uamuzi uliotolewa na Nderitu wa kuunga mkono kutimuliwa kwa Jeremiah Kioni na David Murathe, akidai kuwa chama hicho tayari kilikuwa kimefanyia mabadiliko uongozi wake wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) lililofanyika Jumatatu.

 

Akizungumza wakati wa zoezi la kusambaza chakula kwa waathiriwa wa mafuriko huko Alego Usonga ametaka mabadiliko hayo mapya yafanywe rasmi na mrengo unaoongozwa na Jeremiah Kioni kutambuliwa kama wakuu wa chama cha Jubilee.

 

Nderitu jana Jumanne alithibitisha kuwa Kioni na Murathe wamefurushwa rasmi kutoka kwa chama hicho, akiongeza kuwa timu inayoongozwa na Kanini Kega ndiyo timu halali ya kuongoza shughuli katika chama.

 

Kioni na Murathe walikuwa wameandikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) barua baada ya mrengo wa Jubilee unaoongozwa na Kanini Kega kuwatimua wiki jana.

 

Mzozo katika chama tawala cha zamani kinachoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta umeongezeka baada ya timu ya Kega kuchagua uongozi mpya wa chama.

 

Walimteua mbunge mteule Sabina Chege kama kiongozi wa Jubilee kuchukua nafasi ya Kenyatta.

 

Kioni, Murathe na mweka hazina Kagwe Gichochi walifurushwa kwa misingi ya utovu wa nidhamu, kushindwa kuheshimu kanuni za chama na kutoheshimu makao makuu ya chama.

 

Timu ya Kioni imesalia na msimamo na kusisitiza kuwa kufurushwa na Kega kunakiuka sheria.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!