Home » Kanini Kega Awatimua Murathe Na Kioni

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, ametangaza kuwatimua katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na Makamu Mwenyekiti David Murathe kutoka chama hicho.

 

Kega amesema hayo yanatokana na matokeo ya kamati ya nidhamu iliyosikiliza kesi za Murathe na Kioni.

 

Kulingana na Kega, Kamati ilimpata Kioni na hatia ya mashtaka ya utovu wa nidhamu uliokithiri chini ya Kifungu cha 14(3). Kioni alishutumiwa kwa kutoheshimu sheria za chama.

 

Kioni pia alishindwa kuitisha mkutano wa Halmashauri Kuu ya Kitaifa (NEC) tangu utawala mpya kuchukua mamlaka, kulingana na mrengo wa Kega unaoshirikiana na Rais William Ruto.

 

Mbunge huyo wa EALA pia amesitisha Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) lililoitishwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

 

Kega amebainisha kuwa tarehe rasmi za NDC zitachapishwa baada ya chama hicho kutatua mzozo ambao uliwasilishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya chama.

 

Mrengo wa Kega umeitisha mkutano wa NEC kuweka mikakati ya kukabiliana na NDC iliyopangwa na Uhuru iliyopangwa kufanyika Mei 22.

 

Kufukuzwa kwa Murathe na Kioni kunampa Uhuru pigo lingine ambaye alinyimwa nafasi ya kuandaa mkutano huo huko Bomas huku Uongozi wa Bomas ukieleza kuwa ukumbi huo ulipangwa kufanyiwa ukarabati.

 

Hata hivyo, Kioni alibainisha kuwa wanaandaa ukumbi mwingine kwa ajili ya shughuli hiyo huku wajumbe wakitarajiwa kujulishwa mabadiliko hayo kwa wakati mwafaka.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!