Gavana Ataka Wafugaji Wa Turkana Waliofungwa Uganda Waachiliwe
Gavana wa Turkana Jeremiah Lomorukai ameiomba serikali kuingilia kati kuhusu wakenya 32 waliofungwa nchini Uganda na mahakama baada ya kupatikana na silaha haramu katika eneo la Moroto.
Wakenya hao ambao ni wafugaji kutoka Kaunti ya Turkana, walipatikana na hatia ya kumiliki silaha haramu na mahakama ya taifa hilo na kuwafunga jela kila mmoja kwa miaka ishirini.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kwa maafisa 18 wakuu wa Kaunti ya Turkana, Gavana Lomorukai amemtaka Rais William Ruto kuingilia kati suala hilo ili Wakenya hao warejeshwe humu nchini.
Aidha, Gavana Lomorukai ameapa kuwarejesha wafugaji wote wanaoishi maeneo ya Moroto na Karamoja katika Kaunti ya Turkana.
Kauli yake imeungwa mkono na Spika wa Bunge la Kaunti ya Turkana, Christopher Nakuleu, akizitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumia Sheria kikamilifu huku akikashifu hatua ya Mahakama hiyo ya Uganda kuwafunga raia wa Kenya nchini humo.
Ukame uliwasukuma zaidi ya wafugaji elfu 30,000 kutoka Turkana hadi Uganda kutafuta maji na malisho kwa matumizi ya nyumbani na mifugo.